Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI UWEKEZAJI

Imewekwa: 08 Nov, 2023
SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI UWEKEZAJI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Profesa Godius Kahyrara amesema Serikali itaendelea kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji nchini ili kuboresha sekta ya usafirishaji.

 

Prof. Kahyrara amesema hayo mkoani Morogoro mara baada ya kutembelea Kiwanda cha kutengeneza na kuunganisha ndege ndogo kinachomilikiwa na Kampuni ya Airplane Africa Limited na kusema kuwa uwepo wa kiwanda hiki ni muhimu kwa sasa kwani Serikali inatekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya Anga.

 

“Serikali inaendelea na uwekezaji kwenye sekta ya Anga na uwekezaji huo unafanywa kwa kununua ndege, kujenga miundombinu ya Viwanja lakini pia inazalisha wataalam  katika Nyanja zote za usafiri wa anga, nina imani uwepo wa Kiwanda hiki utawezesha watalaam wetu kupata ajira na kukuza kipato’ amesema  Katibu Mkuu Prof. Kahyarara.

 

Katibu Mkuu Prof. Kahyarara ameipongeza Kampuni ya Czech kwa kuamua kujaa kuwekeza Tanzania kwani sekta ya anga inaendelea kukua kwa kasi baada ya maboresho mbalimbali yanayofanyika.  

 

Aidha, Prof. Kahyarara amevitaka vyuo vilivyo chini ya Uchukuzi kuhakikisha vinazalisha watalaam wenye weledi ili kuiwezesha sekta hiyo kukua zaidi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho Mhandisi Igor Stratl amesema Usalama, utulivu, amani na mazingira wezeshi nchini umeiwezesha Kampuni hiyo kuamua kuwekeza nchini hususani katika uundaji na utengenezaji wa ndege ndogo.

 

Mhandisi Stratl amemuahidi Katibu Mkuu Prof. Kahyarara kiwanda kitaweka kipaumbele kwa watalaam wanaozaliwa katika vyuo vya ndani ya nchi ili kuwaongezea ujuzi na kukuza kipato chao.

 

Kiwanda cha Airplane Africa Limited kilianza mwaka 2021 na mpaka sasa kimeweza kutengeza na kuunganisha ndege zaidi ya tatu ambazo zimeuzwa katika nchi mbalimbali duniani.