Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SERIKALI KUTUMIA BILIONI 435 KUJENGA BANDARI YA MIZIGO MTWARA

Imewekwa: 22 Dec, 2025
SERIKALI KUTUMIA BILIONI 435 KUJENGA BANDARI YA MIZIGO MTWARA

Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao mkoani Mtwara kwa gharama ya shilingi bilioni 435 kwa lengo la kuimarisha usafirishaji na ushughulikiaji wa mizigo ya bidhaa chafu kama makaa ya mawe, saruji, kemikali na mbolea.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa,  tarehe 19 Desemba, 2025 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa mradi huo na  kusisitiza kuwa bandari hiyo imejengwa maalum kwa ajili ya kusafirisha na kupokea bidhaa chafu ambazo awali zilikuwa zikihudumiwa na bandari ya Mtwara

Ameelekeza pia ujenzi wa bandari uende sambamba na ujenzi wa  barabara ya njia nne yenye urefu wa KM 17 kutokana na ongezeko la magari litakalotokana na mradi huo.

Prof. Mbarawa amemhakikishia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Wizara ya Uchukuzi na TPA watatekeleza mradi huo kwa viwango vya juu na kwa kuzingatia thamani ya fedha, kama sehemu ya maono ya Serikali ya kukuza uchumi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, amesema mradi huo uliofikia asilimia 25 ya utekelezaji utaongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara kuhudumia mizigo mikubwa ya kimkakati na kuongeza ushindani wa Tanzania kikanda.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdallah Mwaipaya amesema wamepokea kwa furaha mradi huo na kusisitiza kuwa kukamilika kwake sambamba na barabara za njia nne kutaleta mageuzi makubwa katika shughuli za bandari na maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara

Mradi wa Bandari ya Kisiwa Mgao unatekelezwa na Mkandarasi M/S China Harbour Engineering Company Limited (CHEC) na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2028.