SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI SALAMA NA ENDELEVU KUELEKEA DIRA 2050 – PROF. MBARAWA
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usafiri kwa kuwekeza katika miundombinu bora, nishati safi na teknolojia za kisasa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, nafuu na zenye ufanisi hatua ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani na ustawi jumuishi
Akizungumza katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2026, yanayofanyika Novemba 24 Mlimani City, Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema sekta ya uchukuzi inapaswa kuimarisha usafiri wa umma, kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, kupunguza gharama na muda wa safari pamoja na kuongeza usalama
Aidha, ameipongeza Wizara ya Uchukuzi na LATRA kwa kuunda mfumo wa kidijitali wa kufuatilia magari ya biashara kwa kutumia rasilimali za ndani, akieleza kuwa utasaidia kuimarisha usalama na ufanisi wa usafiri huku akisisitiza matumizi ya nishati safi na uzingatiaji wa malipo ya kielektroniki kwa mujibu wa Amri ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2026
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Bw. Abdallah Mhagama, amesema maadhimisho hayo ni jukwaa la kujadili changamoto na ubunifu katika sekta ya usafiri. Ameeleza kuwa mwaka huu yanatarajiwa kushirikisha washiriki 2,000, ikilinganishwa na 1,200 mwaka 2025
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa CC-TTFA, Dkt. Flory Okonge, amesema ushirikiano na LATRA ni muhimu katika kurahisisha usafiri wa kuvuka mipaka na kuunganisha nchi kupitia Bandari ya Dar es Salaam, barabara na reli, maadhimisho haya yatakayojadili namna ya kupunguza ajali na muda wa safari yatachochea biashara na kuvutia uwekezaji wa kikanda
Naye mwakilishi kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Maria Mapunda amesisitiza ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika kuboresha huduma na kuimarisha usalama wa usafiri
Maadhimisho hayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia tareh 24 - 26, Nov, 2026, yakiongozwa na kaulimbiu ya “Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi”.
