NAIBU WAZIRI KIHENZILE AWATAKA WADAU WA MIUNDOMBINU KUTAFUTA SULUHU ZA AJALI ZA BARABARANI
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), amewataka washiriki wa Kongamano la Usalama Barabarani la Afrika (Africa Road Safety Summit – ARSS 2026) kutumia jukwaa hilo kujadili na kuibua mikakati madhubuti itakayozalisha suluhu za kudumu za kukabiliana na ajali za barabarani na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.
Akizungumza wakati wa kufungua kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Tanzania Road Safety Initiative (TARSI), Novemba 23, 2026, katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam Naibu Waziri Kihenzile amesema ajali za barabarani zinaendelea kuwa changamoto yenye athari kubwa kwa jamii na taifa, ikiwemo kupoteza maisha, kusababisha ulemavu na kuathiri maendeleo ya kiuchumi.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa kukabiliana na changamoto hiyo kunahitaji ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo Serikali, sekta binafsi, wataalamu wa miundombinu, vyombo vya usalama na watumiaji wa barabara, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila, amesema usalama barabarani unahitaji ushirikiano wa karibu katika kuboresha miundombinu, kuimarisha usimamizi na kuongeza elimu kwa watumiaji wa barabara ili kupunguza vihatarishi vinavyosababisha ajali.
Ameeleza kuwa ni muhimu maeneo yanayotokea ajali mara kwa mara kutambuliwa na kufanyiwa tathmini ili kubaini changamoto za kiuhandisi na kuchukua hatua stahiki, ikiwemo kuboresha alama za barabarani na miundombinu inayolenga kulinda watumiaji.
Naye Mkurugenzi wa Tanzania Road Safety Initiative (TARSI), Maliki Barongo, amesema kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri na usalama barabarani kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kupunguza ajali.
Amesema kupitia mijadala hiyo, TARSI inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya wadau na kuhakikisha mawazo na mapendekezo yatakayozalishwa yanasaidia kuweka hatua madhubuti za kuboresha usalama barabarani.
