SERIKALI IMEJIPANGA KUHAMISHA MIZIGO BANDARINI KWA RELI ILI KUONGEZA UFANISI WA BIASHARA NA KUKUZA UCHUMI” PROF.GODIUS KAHYARARA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha sehemu kubwa ya mizigo inayopitia katika Bandari za Tanzania inasafirishwa kwa kutumia reli, hatua itakayoongeza ufanisi wa mfumo wa usafirishaji, kupunguza gharama za usafirishaji na kuwanufaisha wafanyabiashara pamoja na wakulima
Prof. Kahyarara ameyasema hayo wakati wa kuhitimisha ziara yake katika mabanda ya Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake yanayoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, jijini Dodoma
Amesema Serikali, kupitia TPA na TRC, inaendelea kuunganisha kwa ufanisi huduma za bandari na reli ili kuwezesha mizigo kutoka bandarini kusafirishwa kwa haraka na gharama nafuu kwenda maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani, jambo litakaloongeza ushindani wa Bandari za Tanzania na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi
Akizungumzia maendeleo ya usafiri majini, Prof. Kahyarara amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu ya usafiri kwenye Ukanda wa Magharibi, hususan Mkoani Kigoma, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua meli mpya nne za mizigo, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati la kisasa la abiria na mizigo katika Bandari ya Kigoma, pamoja na kushuhudia kukamilika kwa ukarabati mkubwa wa meli ya MV Liemba, ambayo tayari imeanza majaribio kabla ya kurejea kutoa huduma
Prof. Kahyarara amesema miradi hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha usafiri wa majini, kuongeza uwezo wa bandari, kufungua fursa za kiuchumi na kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo ndani ya nchi na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
Aidha, Prof. Kahyarara amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya uchukuzi unaozidi kuiimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji na biashara kikanda.
