Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu azindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala na Uanzishwaji wa huduma ya usafiri wa treni ya mizigo ya reli ya kisasa (SGR)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 31, 2025, amezindua rasmi Bandari Kavu ya Kwala pamoja na kuanzisha huduma ya usafiri wa treni ya mizigo ya reli ya kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma, katika hafla kubwa iliyofanyika Kwala, mkoani Pwani ikihusisha pia upokeaji wa mabehewa mapya 50 ya reli ya zamani MGR na 20 yaliyokarabatiwa na kuweka jiwe la msingi kwenye Kongani ya Viwanda
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Rais Samia amesema mradi huu ni matokeo ya juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kukuza uchumi wa nchi kupitia miundombinu ya kisasa na kuimarisha biashara ya ndani na nje ya nchi.
“Bandari Kavu ya Kwala na huduma ya SGR si tu kwamba zitapunguza msongamano bandarini na barabarani, bali pia zitapunguza gharama za usafirishaji, kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam na kufungua fursa za ajira na biashara kwa Watanzania,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, Mhe. Rais ameipongeza Wizara ya Uchukuzi, TRC, TPA pamoja na wadau wote walioshiriki katika utekelezaji wa miradi hii mikubwa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya kimkakati ili kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati
“Nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa mpya zitakazotokana na miradi hii, kutoka usafirishaji na uhifadhi wa mizigo hadi uendeshaji wa huduma mbalimbali zinazohusiana na bandari,reli na Viwanda,” ameongeza.
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala na huduma za treni ya mizigo ya SGR ni hatua kubwa ya mafanikio katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na dira ya maendeleo ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa Serikali imetenga Shilingi trilioni 2.62 kwa mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya ujenzi na uendelezwaji wa miradi ya miundombinu ya uchukuzi ambapo shilingi Tril 1.51 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya reli ikiwa ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kukuza uchumi wa viwanda nchini