PROF. MBARAWA AMEZITAKA TANROADS,TCAA KUKAMILISHA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE MSALATO MWEZI MEI.
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewataka Wakala wa ,Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuhakikisha kuwa mkandarasi anaejenga kiwanja cha ndege cha Msalato Mkoani dodoma kuongeza kasi kwa kazi zilizobaki kwenye mradi huo ikiwemo jengo la abiria na barabara ya kurukia ndege (runway) ili uanze kutumika ifikapo mwezi Mei Mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa Jijini Dodoma Mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi huo wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato.
“Nitoe Pongezi Kwa hatua zilizofikia kwani Nimeona sehemu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa jengo la abiria ambapo kazi zimefikia asilimia 66.6. Pia ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege (control tower), kituo cha utabiri wa hali ya hewa, na kituo cha zimamoto unaendelea vizuri Kwa upande wa barabara ya kurukia ndege, kazi zimefikia takribani asilimia 96. Kazi inaendelea vizuri na tayari ndege nyingi zilitua hapa wakati wa uapisho wa Mh. Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa Ametoa wito kwa mkandarasi asimamiwe kikamilifu ili akamilishe kazi kwa thamani halisi ya fedha, na kuhakikisha uwekaji wa tiles katika jengo la abiria unafanyika kwa viwango vya juu.
kazi zitakazobaki ni ujio wa magari ya zimamoto pamoja na ukamilishaji wa jengo la abiria, na ifikapo mwisho wa Mwezi Mei Mwaka huu uwanja utakuwa tayari kwa matumizi, jambo ambalo litakuwa na tija kwa nchi na wakazi wa Dodoma.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Eng. Zuhura Amani, amesema wamejipanga kumsimamia mkandarasi huyo ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi wa Kiwanja hicho cha Msalato Clemence Mbaruku, ameongeza kuwa Tutahakikisha ujenzi huo unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa, na tayari watumishi 170 wameshahamia Dodoma kwa ajili ya kuanza kazi mara baada ya uwanja kufunguliwa rasmi, ambapo Mradi huu unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 370.
