PROF. MBARAWA AKUTANA NA KUFANYA KIKAO NA UJUMBE WA BUNGE LA DRC.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amekutana na kufanya kikao na baadhi ya wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) waliopo Nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza.
Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 06 Novemba, 2024 kwenye ukumbi mdogo wa Spika Bungeni Jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine Prof. Mbarawa ameeleza utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana na Nchi jirani katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Wizara ya Uchukuzi pamoja na Taasisi zake inaendelea kusimamia na kudhibiti usafiri na usafirishaji kwa njia ya Anga, Maji, na Ardhi.
Ameongeza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia Dar es Salaam - Mwanza, Kigoma na baadae mpaka Itega Nchini Burundi ambayo inatumia treni ya umeme yenye uwezo wa kusafiri kilometa 160 kwa saa.
Aidha, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa bandari kwenye maziwa yote nchini, maboresho ya viwanja vya ndege, maboresho ya reli ya kati na Tazara ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji ndani na nje ya nchi ambapo ametoa wito kwa Ujumbe huo kuwahimiza wawekezaji kutoka nchini kwao kuchangamkia fursa.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini DRC, Mhe. Said Juma Mshana amesema ujio wa ujumbe huo ni muendelezo wa kuunga juhudi za Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuifungua nchi kimataifa kwa maendeleo endelevu.
Ujumbe huo umeongozwa na Mhe. Balozi wa Tanzania, Mhe. Said Mshana, Mhe. John Banza Lunda - Jimbo la Tanganyika (Kalemie), Mhe. Bosco Pendani - Jimbo la Kivu Kaskazini, Mhe. Enock Nyamwisi -Jimbo la Kivu Kaskazini, Mhe. Tania MOKOLO - Kinshasa, Mje Jethro MUYOMBI - Lubumbashi, Richie MUHOZI-Msaidizi wa Spika, Wakili Joseph Laizer - Afisa Mwandamizi wa Ubalozi na Ellen Maduhu Kaimu Mkurugenzi (DAF) Idara ya Afrika kutoka Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Baadae Wajumbe hao watasafiri kutoka Dodoma kuelekea Dar es salaam kwa kutumia usafiri wa Treni ya Kisasa ya SGR ya Daraja la Kifalme( Royal Class)