PROF. KAHYARARA AMWAKILISHA RAIS SAMIA MKUTANO WA UN

amhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari (Bandari) ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godious Kyaharara anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo unaofanyika Awaza, nchini Turkmenistan tarehe 5-8 Agosti, 2025.
Akifungua Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Turkmenstan Mheshimiwa Serdar Berdimuhamedow amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa, hasa ushirikiano wa nchi za Kusini Kusini katika kukabiliana na changamoto za kipekee zinazozikabili nchi zisizo na bahari na kutoa wito wa ushirikishwaji jumuishi unaohusisha Serikali, mabunge, vijana, na asasi za kiraia.
Alithibitisha msimamo wa Turkmenistan wa kutokuegemea upande wowote na kueleleza kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa maendeleo kwa nchi zisizo na bahari wenye lengo la kukuza miunganisho, ustahimilivu na maendeleo endelevu kwa nchi zisizo na bandari.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. António Guterres, alisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa wenye nguvu na wa vitendo ni muhimu zaidi wakati huu kwa kuwa changamoto za dunia kama za mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kiuchumi, na miundombinu hafifu zinahitaji majibu ya pamoja, hasa kwa nchi zisizo na bahari.
Alitoa wito wa kuwekeza katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2024-2034 wa Awaza na kuongeza kuwa Diplomasia ya usafirishaji ni kiungo muhimu katika kufungua mustakabali wa biashara kwa nchi zisizo na bahari ili kuendeleza maendeleo jumuishi kwa kuwa maendeleo ya nchi hizo ni mafanikio ya dunia nzima na kwamba ustahimilivu wa kijamii na kiuchumi unaweza kufikiwa kupitia mikakati inayojumuisha kila mwananchi wa nchi hizo.
Mkutano huo umeandaliwa na Umoja wa Mataifa, kwa kushirikiana na Serikali ya Turkmenistan unalenga kutathmini utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Vienna kwa Nchi Zisizo na Mlango wa Bahari wa Mpango kazi wa Vienna wa 2014-2024 na kuweka ajenda mpya ya maendeleo jumuishi kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.