Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

PIC YAIPONGEZA SERIKALI KUIMARISHA SEKTA BINAFSI BANDARINI

Imewekwa: 23 May, 2026
PIC YAIPONGEZA SERIKALI KUIMARISHA SEKTA BINAFSI BANDARINI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), ikiongozwa na Mwenyekiti wake Masanja Kadogosa, imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji yanayoendelea kuihusisha sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam na sekta ya uchukuzi kwa ujumla.

Akizungumza baada ya ziara ya kamati hiyo bandarini hapo Mei 23, 2026, Kadogosa amesema maboresho yanayoendelea yameongeza ufanisi na kuipa nafasi sekta binafsi kushiriki moja kwa moja katika kuongeza tija ya shughuli za bandari.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa amesema Serikali imeweka msukumo mkubwa wa ushirikiano na sekta binafsi katika miundombinu ya bandari, reli na usafirishaji ili kuongeza ufanisi na ushindani wa kiuchumi.

Amesema ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka kutoka wastani wa kushughulikia kontena 61,000 hadi zaidi ya 110,000 kwa mwezi, hatua inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi.

Mbarawa ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mipango ya upanuzi wa bandari, ujenzi wa magati 11 na kuimarisha Bandari ya Bagamoyo, huku akisisitiza kuwa ushirikiano na sekta binafsi ndio nguzo kuu ya mafanikio hayo.

Amesema pia maboresho ya miundombinu ya reli ikiwemo TAZARA yanalenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kutoka nchi jirani, hatua itakayoiweka Tanzania katika ushindani mkubwa wa kikanda dhidi ya bandari za Mombasa na Durban.