Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MITAWI AMTAKA MKANDARASI KUFIDIA MUDA ULIOPOTEA KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA

Imewekwa: 29 Oct, 2026
MITAWI AMTAKA MKANDARASI KUFIDIA MUDA ULIOPOTEA KIWANJA CHA NDEGE KIGOMA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. Abdallah Mitawi, amemtaka mkandarasi wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege Kigoma Kampuni ya CRCEG,kutoka China kuweka mkakati madhubuti wa kufidia muda uliopotea na kuongeza kasi ya kazi bila kuathiri ubora, agizo ambalo amelitoa wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo tarehe 28 Oktoba,2026

Mitawi amesisitiza umuhimu wa kuandaa ratiba mahsusi ya kukamilisha kazi zilizobaki, kuongeza nguvu kazi na kuimarisha usimamizi ili mradi ukamilike kwa wakati na viwango vinavyotakiwa

Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, Bw. Daniel Mbura, amebainisha changamoto za kuongezeka kwa viwango vya kazi na athari za mabadiliko ya tabianchi, zinazosababisha maji kuingia uwanjani na kusisitiza umuhimu wa kupata suluhisho la kudumu kulinda miundombinu na usalama wa shughuli za anga

Awali, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mha. Elisony Mweladzi, amesisitiza kuzingatiwa kwa viwango vya ujenzi na kuboreshwa kwa mifumo ya kuondoa maji ili kuhakikisha uimara na ubora wa miundombinu

Mradi huo umefikia asilimia 77 ya utekelezaji, huku mkandarasi akiwa amelipwa jumla ya Sh bilioni 23.2. Kukamilika kwake kunatarajiwa kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuchochea biashara, uwekezaji na utalii kikanda.