TRC YATUMIA SIMULATOR KUIMARISHA USALAMA WA UENDESHAJI WA TRENI – PROF. MBARAWA
Shirika la Reli Tanzania (TRC) linatumia teknolojia ya kisasa ya mafunzo ya udereva wa treni (Simulator) kuimarisha usalama wa usafiri wa reli nchini kwa kuwajengea madereva uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa safari.
Akizungumza mkoani Mwanza, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kifaa hicho kinawezesha madereva kujifunza uendeshaji wa treni katika mazingira yanayofanana na hali halisi, ikiwemo njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Amesema simulator hiyo huonesha mazingira mbalimbali ya safari, yakiwemo kona na hitilafu zinazoweza kujitokeza kwenye njia ya reli, hivyo kuwasaidia madereva kutambua changamoto mapema na kujifunza namna sahihi ya kukabiliana nazo ili kulinda usalama wa abiria, mizigo na treni.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema Serikali inatarajia kujenga chuo cha mafunzo ya udereva wa treni kwa lengo la kuongeza idadi ya madereva wenye ujuzi unaohitajika katika sekta ya reli. Kuhusu Stesheni ya Seke mkoani Shinyanga, amesema maeneo ya abiria wanaoanza safari na wanaowasili yatatenganishwa, pamoja na maeneo ya tiketi, ili kupunguza msongamano na kurahisisha huduma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, amesema shirika hilo linaendelea kuimarisha uwezo wa kiutendaji kwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kuwajengea wafanyakazi ujuzi unaohitajika ili kuongeza ufanisi na usalama wa huduma za reli.
Ameongeza kuwa TRC inaendelea na mipango ya kununua mitambo ya matengenezo ya miundombinu, vichwa vya treni za umeme, treni za abiria na vifaa vingine muhimu kwa ajili ya Reli ya Kisasa (SGR), hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa shirika kutoa huduma bora na za uhakika kwa usafiri wa abiria na mizigo.
