Naibu Waziri Kihenzile azitaka taasisi kuweka mikakati ya utendaji inayotekelezeka

Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Mhe. David Kihenzile amezitaka taasisi zilizopo chini ya Wizara kuongeza kasi ili kufikia malengo waliojiwekea ikiwa ni pamoja na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoko chini yao kwa wakati na thamani halisi ya fedha.
Kihenzile ameyasema hayo leo tarehe 25 Oktoba,2024 wakati akifuga mkutano wa 17 wa tathmini ya utendaji wa Wizara ya Uchukuzi uliofanyika Kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha(AICC)
“Wizara ya Uchukuzi ni injini muhimu ya maendeleo ya Taifa lolote ,Uchumi wa kisasa hauwezi kuimarika bila kuwa na mifumo ya usafiri iliyo bora, inayotegemeka na ya kisasa,”amesema Kihenzile
Kihenzile amesema lengo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuboresha miundombinu yote nchini ikiwemo ya Uchukuzi ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi.
Naibu Waziri Kihenzile amewataka washiriki wote kutoka idara , taasisi na wadau wa Usafirishaji nchini kuhakikisha wanaiweka mipango na mikakati iliyojadiliwa kwenye utekelezaji ili kufikia ufanisi uliokusudiwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof Godius Kahyarara kupitia Mkutano huo masuala muhimu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo kama ujenzi wa meli, reli ya SGR, maboresho na upanuzi wa bandari, ununuzi wa ndege, miundombinu ya vyuo vya usafirishaji, umuhimu wa mabadiliko ya sera ya uchukuzi yamekamilika kwa mawanda yake.
Naye muwakilishi kutoka sekta binafsi Mha. Munina Wakyendo amesema Wizara ya Uchukuzi ni kichocheo muhimu kwa kuinua sekta zingine na uchumi hivyo vikao vya maboresho na majadiliano vitawasaidia wawekezaji kujua fursa za kuwekeza kwa kuwa na uhakika wa kutatuliwa changamoto zao na kuahidi kuendelea kufadhiri miradi ya kimkakati nchini.