Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Naibu Waziri Kihenzile ataka Bodi TMA kukamilisha Miradi

Imewekwa: 13 Feb, 2026
Naibu Waziri Kihenzile ataka Bodi TMA kukamilisha Miradi

Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ameitaka bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na menejimenti kusimia na kuhakikisha miradi ya ujenzi wa jengo la Kituo cha Taifa cha Urekebishaji Vifaa vya Hali ya Hewa na ujenzi wa jengo la Kituo cha Utoaji Taarifa za Majanga ya Tsunami Kanda ya Mashariki unakamilika katika ubora na kwa wakati.

Kihenzile ameyasema hayo leo alipotembelea miradi hiyo inayotekelezwa kwa wakati mmoja katika jiji la Dar Es Salaam, ambapo miradi hiyo inatarajiwa kuleta ufanisi mkubwa katika utabiri wa hali ya hewa nchini mara itakapokamilika.

“Sisi kama serikali tutahakikisha tunasukuma na kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati lakini na ninyi kwa upande wenu simamieni ipasavyo ili kazi ifanyike kwa ubora na kiwango kinachotakiwa,” Ameongeza Kihenzile.

Aidha Kihenzile amesema kuwa majengo yote mawili yanakwenda kuongeza thamani katika taarifa za utabili wa hali ya hewa pamoja na kuwapa fursa wataalamu kutimiza majukumu yao katika mazingira mazuri.

Awali akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo Mshauri Mwelekezi wa Mradi Mhandisi Dkt. Johnson Malisa amesema kuwa ujenzi wa jengo la Kituo cha Utoaji Taarifa za Majanga ya Tsunami Kanda ya Mashariki unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 9.9 na mpaka sasa umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026.

Kwa upande wa mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo cha Taifa cha Urekebishaji Vifaa vya Hali ya Hewa amesema mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.6 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 31 za ujenzi wake na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.