NAIBU WAZIRI KIHENZILE ASHIRIKI MKUTANO WA NGAZI YA MAWAZIRI WA TANZANIA NA ZAMBIA
Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile ameshiriki katika Mkutano wa Tano wa Kamati ya Pamoja ya Biashara (5th Joint Trade Committee - JTC) kati ya Tanzania na Zambia kwa ngazi ya mawaziri uliofanyika katika mpaka wa Tanzania na Zambia mjini Tunduma mkoa wa Songwe.
Mkutano huo uliohusisha mawaziri kutoka Tanzania na Zambia umejadili na kutoa maamuzi kwenye masuala mbalimbali yanayohusu biashara baina ya nchi ya Tanzania na Zambia ikiwa ni pamoja na kupitia utekelezaji wa masuala yaliyokubalika katika mkutano wa nne na masuala mapya yaliyojitokeza baadaye.
Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha siku mbili kwa ngazi ya wataalamu kwa nchi zote mbili, na kufuatiwa kwa kikao cha siku moja kwa ngazi ya makatibu wakuu na hatimaye kuhitimishwa kwa mkutano ngazi ya mawaziri.
Mawaziri waliohudhuria katika mkutano huo ni Naibu Waziri wa Fedha Mshamu Ali Munde, Naibu Waziri Viwanda na Biashara Dennis Londo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Millya na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Mwakiposa Kihenzile huku Zambia ikiwakilishwa na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia, Njavwa Simutowe.
