NAIBU KATIBU MKUU NDUHIYE ITAKA TAA KUKITANGAZA KIWANJA CHA NDEGE MTWARA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameutaka uongozi wa Kiwanja cha Ndege Mtwara kuisaidia serikali kwa njia ya kuwajibika na kutangaza mafanikio yanayopatikana katika kiwanja hicho.
Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea kiwanja hicho ambacho kimefanyiwa maboresho huku maboresho zaidi yakitarajiwa kufanyika.
Nduhiye amepongeza maendeleo yaliyofanyika katika kiwanja hicho ikiwa ni pamoja na uwezo wa kiwanja hicho kufanya kazi saa 24, huku akisisitiza kuwepo kwa jitihada za makusudi ili kuvutia abiria ili kuongeza miruko zaidi.
Meneja wa kiwanja hicho Jordan Mchami amesema kiwanja hicho kina uwezo wa kuhudumia ndege wakati wa usiku pamoja na wakati wa hali inayosababisha uoni hafifu na hii ni kutokana na kuwepo kwa taa za kuongozea ndege.
Aidha Mchami amesema katika awamu ya kwanza ya uboreshaji na upanuzi wa kiwanja hicho serikali imefanikisha kujengwa kwa njia ya kurukia ndege yenye urefu wa mita 2800 na upana wa mita 45 kwa kiwango cha lami.
Pia amesema kuwa wamefanikiwa kujenga eneo la maegesho ya ndege, barabara ya kiungio (Taxiway) yenye urefu wa mita 467 pamoja na ujenzi wa barabara mpya ya magari kuingia uwanjani hapo.