Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

NAIBU KATIBU MKUU NDUHIYE ATAKA MATOKEO UENDESHAJI VIWANJA VYA NDEGE

Imewekwa: 31 Oct, 2024
NAIBU KATIBU MKUU NDUHIYE ATAKA MATOKEO UENDESHAJI VIWANJA VYA NDEGE

aibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Abdul Mambokaleo kuwa na maono makubwa kwa ajili ya uendelezaji wa viwanja vya ndege nchini na kutengeneza ushawishi wa anaowaongoza ili kupata uungwaji mkono.

 

Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea makao makuu ya taasisi hiyo yaliyopo jijini Dar Es Salaam na kukutana na menejimenti, kwa lengo la kujua maendeleo ya taasisi hiyo kiutendaji pamoja na mikakati iliyopo katika kujiendeleza.

 

" Ni vema ukawa na maono makubwa ambayo utawashirikisha hawa, hata kama watakuwepo watakao kushangaa kwa kutokukuelewa basi wawe ni wachache kabisa," Amesema Nduhiye.

 

Aidha Naibu Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa matumizi bora ya teknolojia katika utendaji kwa kile alichoeleza kuwa matumizi teknolojia kwa sasa si jambo la hiyari bali ni lazima maana dunia inataka hivyo.

 

Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Abdul Mambokaleo amesema kuwa TAA inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha huduma katika viwanja vya ndege zinakuwa za kuridhisha ili kuvutia mashirika mengi zaidi hatimaye kuboresha huduma za usafiri.

 

Kwa upande wake Meneja Mipango na Takwimu Nasib Elias, amesema TAA imeendelea kupiga hatua, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita imeweza kushuhudia ongezeko la safari za ndege kwa asilimia tatu, ongezeko la tani za mizigo kwa asilimia tano na ongezeko la abiria ikiwa ni asilimia 9 huku Mkoa wa Arusha ukiwa na rekodi ya ongezeko kubwa zaidi la abiria.

 

Elias amesema pia katika kipindi hicho TAA imefanikiwa kuvutia mashirika matatu ya ndege kutoka Saudi Arabia, Ufaransa na Zambia jambo ambalo ni matokeo ya ufanisi na ubora uliopo katika utendaji.