Naibu Katibu Mkuu Nduhiye asisitiza Ushirikiano Taasisi za Uchukuzi
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye amezitaka taasisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi katika sekta ya Usafiri wa Anga nchini.
Nduhiye ameyasema hayo alipotembelea Kiwanja cha Ndege cha Arusha kwa lengo la kujionea maendeleo ya kiwanja hicho huku akipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Mameneja wa taasisi zote nne.
“Niwaombe mfanye kazi kwa pamoja kama mafiga manne na kutatua matatizo kwa pamoja ili kufikia lengo kama nchi, kwani serikali imewekeza kwenye mifumo muitumie vizuri na kuitunza,” Amesema Nduhiye.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha Godfrey Parmena amesema kuwa ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja hicho umefikia asilimia 95 na limeanza kutumika tangu Septemba 9 huku likitarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Aidha Parmena amesema kuwa serikali Katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 7 kwa ajili ya usimikaji wa taa za kuongozea ndege jambo litakalowezesha ndege kuruka na kutua wakati wa usiku.
TMA na TCAA wameishukuru Serikali kwa kuwezesha ufungwaji wa mifumo ya kisasa ya kuongozea ndege na mifumo kwa ajili ya uangazi na utabili wa hali ya hewa.