NAIBU KATIBU MKUU NDUHIYE AITAKA TPA KUITANGAZA BANDARI YA MTWARA

Naibu katibu Mkuu wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika Bandari ya Mtwara, kuhakikisha inapambana usiku na mchana kuleta ufumbuzi namna ya kupata mzigo zaidi wa kulisha bandari hiyo kutoka bandari ya Mbamba bay, nchi ya Zambia, Malawi na ukanda wote wa SADC.
Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea bandari hiyo iliyo kusini mashariki mwa Tanzania ukiwa ni muendelezo wa ziara katika bandari mbalimbali, lengo likiwa ni kujionea utendaji kazi na maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo.
“Unajua bandari hii ni mlango wa SADC, mnaweza kuwa na mabalozi wenu ambao ni wataalamu kwa ajili ya kupambana kupata mzigo zaidi na kuvutia wateja kutoka nchi za SADC ili kuongeza ufanisi wa bandari yenu,” Amesema Nduhiye.
Aidha Nduhiye ameitaka mamlaka hiyo kutojiwekea malengo madogo kwani kufanya hivyo kunaweza kusiwe na tija kubwa huku akisisitiza kuwa kuweka malengo ya kile kinachoonekana na wengi kuwa hakiwezekani ni njia sahihi ya kufikia malengo makubwa na yenye tija.
Kwa upande wake Meneja wa bandari Ferdinand Nyathi amesema bandari hiyo imeendelea kufanya vizuri katika kuhudumia shehena ambapo mwaka 2021/22 bandari hiyo ilihudumia mzigo wa tani 512,000 huku katika mwaka 2024/2025 ( Julai – Desemba 2024) ikiwa imehudumia tani milioni 1.4 ikiwa ni nusu mwaka na lengo likiwa ni kufikia tani 1.7 jambo linalotoa uhakika kuwa wanaweza kuzidi lengo kwa kipindi cha nusu mwaka kilichosalia.
Pia Nyathi amesema kuwa kwa mwezi Julai – Desemba wameweza kuhudumia meli 122 huku lengo likiwa ni meli 320 ifikapo mwisho wa mwaka, pia katika mapato bandari hiyo katika mwaka wa fedha 2022/23 iliweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 36 na mwaka huu 2024/25 (Julai – Desemba 2024) imeweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 44 na matarajioni ni kufikia bilioni 60 hadi 70 ifikapo mwisho wa mwaka.