NAIBU KATIBU MKUU NDUHIYE AIPONGEZA TPA TANGA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kufanya kazi kubwa ya kuzifanya bandari kuwa na ufanisi na zinazokua kila siku kiutendaji na kimapato moja wapo ikiwa ni Bandari ya Tanga.
Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea Bandari ya Tanga ili kujionea utendaji kazi pamoja na kujua changamoto mbalimbali zinazoikabiri bandari hiyo ambayo imefanyiwa maboresho makubwa hivi karibuni.
“Tunamshukuru mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kusaidia TPA kuweza kubaki na mapato yake ya ‘wharfage’, hivyo mnayo kazi kubwa ya kuionyesha serikali kuwa haikufanya makosa kufanikisha jambo hilo licha ya changamoto ya kisheria iliyokuwepo,” Amesema Nduhiye.
Aidha Nduhiye amesisitiza umuhimu wa TPA kuangazia changamoto zinazosababisha mzigo mwingi wa chi za Uganda, Rwanda na Burundi kupita bandari ya Mombasa – Kenya badala ya Bandari ya Tanga, na kubainisha kuwa endapo changamoto hizo zitatatuliwa bandari hiyo inaweza kuhudumia mzigo wa nchi hizo kwa kiasi kikubwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Bandari ya Tanga Meneja wa bandari hiyo Masoud Mrisha, amesema ujenzi wa gati na kuongezwa kwa kina cha bahari pamoja na ununuzi wa vifaa katika bandari hiyo kumesaidia kuongeza ufanisi kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuhudumia mzigo mkubwa kwa muda mfupi na gharama ndogo jambo linalovutia wateja wengi Zaidi.
Mrisha amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano yani 2019/20 hadi 2023/24 kiwango cha shehena iliyohudumiwa kimekuwa kikiongezeka kwa wastani wa asilimia 27.2 kwa mwaka kwani shehena imeongezeka kutoka tani za uzito 470,611 mwaka 2019/20 hadi tani 1,191,480 mwaka 2023/24.
Pia Mrisha amesema kuwa kwa kipindi cha miezi sita kwa mwaka wa fedha 2024/25 Julai – Desemba 2024 mapato yaliyokusanywa ni bilioni 45.69 ikiwa ni sawa na asilimia 200.48 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 22.79.