Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Naibu Katibu Mkuu Nduhiye aipongeza TMA

Imewekwa: 13 Nov, 2024
Naibu Katibu Mkuu Nduhiye aipongeza TMA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa ufanisi mkubwa katika kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

 

Nduhiye ametoa pongezi hizo alipotembelea makao makuu ya TMA jijini Dar Es Salaam ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na menejimenti ikiwa ni pamoja na kupokea taarifa ya utendaji.

 

“Ni lazima tuseme ukweli TMA hii siyo ile ya zamani ambapo yaliyokuwa yakitabiriwa yalikuwa yanatokea kwa asilimia chache lakini sasa hivi lolote mnalolisema linatokea hivyo tunalazimika kufanyia kazi utabiri wenu, “ Amesema Nduhiye.

 

Pamoja na hayo Nduhiye amesema mamlaka hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa kwenye teknolojia ili kuendelea kuwa na ufanisi unaotakiwa jambo ambalo serikali imeonesha nia yankufanya hivyo.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt.Ladslaus Chang’a ameishukuru serikali kwa jitihada inazoendelea kufanya ikiwa ni pamoja na kupeleka wataala kwenda nje kusoma ambapo kwa sasa zaidi ya watanzania 12 wako nchini china kusomea mambo ya hali ya hewa.

 

Aidha Dkt.Chang’a amebainisha mafanikio mbalimbali ya TMA ikiwa ni pamoja na kuteuliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuwa mratibu wa ubora wa data kwa vituo vya Afrika Mashariki na kufanikiwa kuandaa mkutano wa mafunzo kwa nchi 12 barani Afrika huku wakufunzi wakitoka TMA.

 

Pia Dkt.Chang’a amesema kuwa TMA imekuwa ikihusika kikamilifu katika miradi ya kimkakati ili kuhakikisha haiathiriwi na changamoto za hali ya hewa ambapo ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na SGR, Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere pamoja na mradi wa Bomba la mafuta kati ya Tanzania na Uganda.