Naibu Katibu Mkuu Nduhiye aipongeza TCAA

Serikali kupitia Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye imeipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa maono makubwa na ufanisi katika utendaji huku Mamlaka hiyo ikitakiwa kujua kuwa inayo nafasi kubwa katika kukuza uchumi nchini.
Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea makao makuu ya taasisi hiyo jijini Dar Es Salaam ikiwa ni muendelezo wa ziara zake kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi, ili kujionea utendaji kazi pamoja na mikakati iliyopo.
"Mmewahi kufikiri huduma za usafiri wa anga zisitishwe nchini kwa ghafla, changamoto yake itakuwa kubwa. pia mnatakiwa kujua mmechangia ongezeko la watalii nchini hiyo iwape kuona uthamani mlionao, " Amesema Nduhiye.
Aidha Nduhiye amewataka kujipanga vizuri kwani sekta hiyo ya usafirishaji ni ya msingi hususan kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki kutokana na uwekezaji mkubwa ambao serikali imeendelea kuufanya.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Salim Msangi amesema kuwa taasisi hiyo imepiga hatua kubwa ukilinganisha na hapo awali kwani kwa sasa linaweza kudhibiti anga la Tanzania kwa asilimia 100 baada ya kufunga rada nne (4) kwani awali ilikuwepo rada moja (1) na iliyokuwa na uwezo wa kudhibiti anga kwa asilimia 25 pekee.
Pia Msangi amesema kuwa TCAA inakusudia kujenga chuo cha kisasa cha mafunzo ya mambo ya anga ili kuongeza wataalamu wengi zaidi wazawa na kuongeza ufanisi katika sekta hiyo nchini.