Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

NAIBU KATIBU MKUU AITAKA ATCL KUWEKA MKAKATI WA KUONGEZA ABIRIA KIGOMA

Imewekwa: 09 Sep, 2025
NAIBU KATIBU MKUU AITAKA ATCL KUWEKA MKAKATI WA KUONGEZA ABIRIA KIGOMA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameutaka uongozi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Mkoa wa Kigoma kufanya jitihada za kuhakikisha abiria wanaongezeka siku za usoni, pale maboresho ya kiwanja cha ndege Kigoma yatakapokamilika.

Nduhiye ameyasema hayo leo alipotembelea kiwanja hicho mkoani Kigoma ili kujionea maendeleo ya mradi wa upanuzi na maboresho ya kiwanja unaohusisha ujenzi wa jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege pamoja na maegesho ya ndege (apron).

“ Kama baada ya kiwanja kukamilika kinaweza kuhudumia abiria mpaka laki nne (400,000) kwa mwaka unadhani abiria hao watakuja wenyewe?, nikuombe meneja usilale wekeni mkakati wa namna ya kuongeza abiria maana Kigoma iko sehemu nzuri,” Amesema Nduhiye.

Aidha Naibu Katibu Mkuu amebainisha kuwepo kwa fursa ya kupata abiria kutoka nchi jirani za DR Congo na Burundi huku akieleza kuwa mpaka sasa raia wa Burundi wamekuwa wakitumia usafiri wa ATCL hivyo jitihada zikifanyika abiria watakuwa wengi zaidi.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Kaimu Mhandisi Mkaazi wa Mradi Dadi Shahame, amesema mpaka sasa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 51.4 umefikia asilimia 31  ukihusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria, upanuzi wa maegesho ya ndege, uzio wa uwanja, mnara wa kuongozea ndege na taa za kuongozea ndege.

Kwa upande wake Meneja wa ATCL Mkoa wa Kigoma Mwantumu Kipwasa amesema kuwa kukamilika kwa maboresho ya kiwanja hicho kutasaidia ongezeko la abiria hususani wafanyabiashara kutoka nchi jirani za DR Congo, Rwanda na Burundi.