MTANDAO WA SAFARI ATCL WAONGEZEKA
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limeanzisha rasmi safari ya moja kwa moja kutoka jijini Dar Es Salaam hadi visiwa vya Shelisheli katika uzinduzi uliofanyika leo Mei 3, 2026 ukiongozwa na Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa.
Uzinduzi huo umeambatana na safari ya kwanza iliyofanyika kutoka jijini Dar Es Salaam kwenda Visiwa vya Shelisheli, huku baadhi ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakishiriki wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Selemani Kakoso.
Katika hotuba ya uzinduzi visiwani humo Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa, kuanza kwa safari hizo kutajenga daraja litakalounganisha masoko, watu na fursa za kiuchumi kati ya nchi zote mbili.
“Safari hii itapunguza gharama za kusafiri kutoka Dar Es Salaam hadi Visiwa vya Shelisheli lakini pia itaongeza urahisi wa usafiri kwa watalii na wafanyabiashara,” Ameongeza Mbarawa.
Awali akizungumza katika salamu za ukaribisho Katibu Mkuu wa Usafiri wa Anga, Bandari na Usafiri kwa njia ya Maji wa nchini humo David Bianchi amesema kuwa kuanza kwa safari hizo kuanzisha hatua mpya ya ushirikiano katika eneo hili kupitia bahari ya hindi.
Aidha David amesema kuwa jambo hili litahamasisha kupatikana kwa abiria wengi zaidi na hatimaye kunufaika katika utalii na uzoefu mpya wa kiutamaduni baina ya nchi zote mbili.
