MKUTANO WA MAWAZIRI WA UCHUKUZI TANZANIA, BURUNDI NA DRC WAWEKA MSINGI IMARA WA MRADI WA SGR
Mkutano wa Mawaziri wa Uchukuzi kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umehitimishwa rasmi jijini Kinshasa, ukiweka msingi imara wa kuharakisha utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya umeme (SGR) unaotarajiwa kubadilisha mwelekeo wa uchumi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mkutano huo uliofanyika tarehe 31 Machi 2026 uliwakutanisha viongozi wakuu wa sekta ya uchukuzi kutoka nchi hizo tatu, wakiongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchukuzi wa DRC, Mhe. Jean-Pierre Bemba Gombo.
Katika mkutano huo, mawaziri walipitisha rasmi ripoti ya maendeleo ya upembuzi yakinifu wa kipande cha reli ya SGR kutoka Msongati hadi Kindu, ikiwa ni sehemu ya mradi mpana unaounganisha reli kutoka Tanzania kupitia Burundi hadi mashariki mwa DRC. Hatua hiyo imeelezwa kuwa muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Mradi wa reli ya SGR unatarajiwa kuunganisha miji ya Uvinza, Musongati, Gitega, Bujumbura, Uvira hadi Kindu, na hivyo kurahisisha usafirishaji wa Shehena na abiria kati ya nchi hizo. Reli hiyo pia itakuwa kiungo muhimu kati ya nchi zisizo na bandari na Bandari ya Dar es Salaam, ambayo imeendelea kuwa lango kuu la biashara kwa ukanda huo.
Takwimu zinaonesha kuwa DRC inaongoza kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa na zaidi ya tani milioni 5.9 za mizigo zilizopitishwa katika mwaka wa fedha 2024/25. Hali hiyo inaifanya DRC kuwa mshirika muhimu wa kibiashara kwa Tanzania, huku matarajio yakiwa ni kuongezeka zaidi kwa biashara kupitia mradi huo wa SGR.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Godius Kahyarara alisisitiza kuwa mradi huo ni zaidi ya miundombinu ya usafiri, bali ni chachu ya maendeleo ya pamoja kwa nchi za ukanda. Alieleza kuwa utekelezaji wake utaongeza kasi ya biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kimataifa.
Kwa upande wao, mawaziri kutoka Burundi na DRC walieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa, wakiahidi kuendelea kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati. Pia walikubaliana kuharakisha kukamilika kwa tafiti zilizobaki na kuimarisha uratibu kupitia taasisi ya ukanda inayosimamia usafirishaji.
Kwa ujumla, mkutano huo umeonesha dhamira ya dhati ya nchi tatu katika kujenga miundombinu ya kisasa itakayounganisha masoko, kuchochea biashara na kuleta maendeleo ya pamoja kwa wananchi wa Afrika Mashariki na Kati.
