Mkataba wa TAZARA wasainiwa Nchini China

Hatua kubwa ya kihistoria imefikiwa 29 Septemba 2025 nchini China baada ya Serikali ya Tanzania, Zambia na China kusaini mkataba wa kufufua reli ya TAZARA, ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa uti wa mgongo wa biashara kati ya Afrika Mashariki na Kusini mwa bara la Afrika.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa, amezishukuru Serikali zote tatu kwa mshikamano na dhamira ya dhati ya kuhakikisha TAZARA inarejea katika ubora wake.
Waziri Prof. Mbarawa pia ametumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Mheshimiwa Rais Hakainde Hichilema wa Zambia, kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha hatua hiyo muhimu ya uhai mpya wa shirika hilo la reli.
Waziri huyo alibainisha kuwa kufufuliwa kwa TAZARA kutakuwa na manufaa makubwa, yakiwemo Kuimarisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na nchi nyingine wanachama wa SADC,Kupunguza gharama na muda wa usafirishaji, Kuchochea biashara ya kikanda na kuvutia wawekezaji, Kuongeza ajira na kipato kwa wananchi, Kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania, Zambia na China.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi na Usafirishaji wa Zambia, Mhe. Frank Tayali, alisema mkataba huo umesainiwa kwa wakati muafaka, na mara baada ya maboresho kukamilika, reli hiyo itaimarika zaidi na kupanua wigo wa usafirishaji wa abiria na mizigo kwa nchi zinazotegemea huduma za treni.
Reli ya TAZARA, iliyojengwa miaka ya 1970 kwa ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania, Zambia na China, imekuwa mhimili muhimu wa uchumi wa kikanda. Kufufuliwa kwake kunatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kukuza biashara, ajira na maendeleo ya kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kusini.