MITAWI AITAKA TPA KUHARAKISHA MIRADI YA BANDARI ZA ZIWA TANGANYIKA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Abdallah Mitawi, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha miradi ya maendeleo katika bandari za Ziwa Tanganyika inatekelezwa kwa kuzingatia ubora, thamani ya fedha na muda uliopangwa. Amesema uwekezaji huo ni muhimu katika kuboresha huduma za usafirishaji, kukuza biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi
Mitawi ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Bandari ya Kigoma, mkoani humo ambapo katika ziara hiyo, alikagua ujenzi wa gati na jengo la kuhudumia abiria, gati la mizigo, maboresho ya Bandari ya Kibirizi na Bandari Kavu ya Katosho
Amesisitiza kuwa miundombinu hiyo inapaswa kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta ya usafirishaji na kuelekeza usimamizi madhubuti wa miradi ili kuhakikisha rasilimali zinazotumika zinaleta tija iliyokusudiwa
Mitawi alieleza kuwa bandari za Ziwa Tanganyika zina nafasi ya kimkakati katika kuunganisha Tanzania na nchi jirani, kurahisisha usafirishaji wa mizigo na kuongeza fursa za biashara za kikanda na kusisitiza umuhimu wa kutafuta suluhisho za changamoto za ufinyu wa maeneo ya bandari, uhaba wa meli kubwa za kibiashara na athari za mabadiliko ya tabianchi
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Bi. Jocelyne Sima, alisema ujenzi wa gati na jengo la kuhudumia abiria katika Bandari ya Kigoma unaogharimu shilingi bilioni 39 unatarajiwa kukamilika Novemba 2027 mradi ambao utaboresha huduma na mazingira ya usafiri wa majini
Kuhusu gati la mizigo, Bi. Sima alisema ujenzi wake ulianza mwaka 2026 na unatarajiwa kuchukua miezi 24 mradi ambao utaongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo na kuimarisha ufanisi wa shughuli za kibiashara
Aidha, alisema uboreshaji wa Bandari ya Kibirizi unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bil.37, huku uwepo wa Bandari Kavu ya Katosho ukiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji maboresho ambayo yatarahisisha mtiririko wa mizigo na kuongeza ufanisi wa huduma katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
