Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MBARAWA AKAGUA UJENZI WA MATANGI YA MAFUTA KIGAMBONI

Imewekwa: 28 Nov, 2025
MBARAWA AKAGUA UJENZI WA MATANGI YA MAFUTA KIGAMBONI

WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amekagua maendeleo ya ujenzi wa matangi 15 ya kuhifadhia mafuta yanayotekelezwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa gharama ya Sh bilioni 703 katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam.

Mradi huo ulioanza Agosti 2024 na unatarajiwa kukamilika Agosti 2026 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 33.57 na ujenzi wa misingi na nguzo muhimu za matenki ukiwa umekamilika.

Profesa Mbarawa amesema matanki hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 378,000 na yatapunguza foleni za meli za mafuta pamoja na gharama za uingizaji.

Amesema baada ya mradi kukamilika, muda wa meli kushusha mafuta utapungua kutoka siku saba hadi siku tatu au nne, hatua itakayopunguza gharama kwa waingizaji na kufanya mafuta kupatikana kwa bei nafuu.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Dk. Baraka Mdima, alisema kazi inaendelea kwa kasi na maandalizi ya msingi wa matenki yamekamilika, huku awamu nyingine zikiendelea kama ilivyopangwa.