Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Mashirika ya Ndege Yatakiwa Kutumia Fursa ya Uwanja wa Katavi

Imewekwa: 24 Feb, 2026
Mashirika ya Ndege Yatakiwa Kutumia Fursa ya Uwanja wa Katavi

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ametoa rai kwa mashirika binafsi ya ndege kuanza kutoa huduma katika Uwanja wa Ndege wa Katavi kufuatia kukamilika kwa maboresho yaliyoongeza uwezo wa kiwanja hicho kuhudumia abiria na ndege zaidi.

Akizungumza wakati alipotembelea Kiwanja cha Ndege cha  Katavi, Naibu Waziri Kihenzile amesema shughuli za madini, utalii na biashara zimechochea mahitaji makubwa ya usafiri wa anga, hivyo ni muhimu kwa mashirika mengine ya ndege kutumia fursa hiyo kuanzisha safari za moja kwa moja kupitia Kiwanja hicho.

“Maboresho yaliyofanyika katika Kiwanja hiki yameongeza idadi ya abiria na kuimarisha hudum na kwa sasa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) pekee ndio  linalotoa  huduma na linafanya safari mara tatu kwa wiki hivyo Ni wakati muafaka kwa mashirika mengine kuangalia fursa iliyopo Katavi,” amesema Naibu Waziri  Kihenzile.

Aidha,Naibu Waziri Kihenzile amempongeza Meneja wa Uwanja huo, Fadhili Magehema, kwa kusimamia vyema maboresho na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usafiri wa anga vilivyowekwa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO).

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafiri wa anga hususani jengo kubwa la abiria  hatua iliyopunguza msongamano wa abiria na kuongeza ufanisi wa huduma.

Meneja wa Uwanja huo Fadhili Magehema, amesema kukamilika kwa maboresho ya Kiwanja hicho yameongeza idadi ya abiria kutoka 15,219 mwaka 2024 hadi 15,700 mwaka 2025, huku ndege zilizohudumiwa zikiongezeka kutoka 197 mwaka 2024 hadi 234 mwaka 2025  jambo linaloashiria kukua kwa shughuli za usafiri wa anga mkoani humo.