Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA) YATAKIWA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO.

Imewekwa: 18 Dec, 2025
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA) YATAKIWA KUBUNI  VYANZO VIPYA VYA MAPATO.

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, tarehe 18 Desemba, 2025 amefungua  Mkutano wa 34 wa Baraza la Wafanyakazi wa TAA unaofanyika katika Ukumbi wa CATE Hotel, Mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano hu ,Prof. Mbarawa amewapongeza wafanyakazi wa TAA kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu, nidhamu kazini na ushirikiano kati ya Uongozi  na wafanyakazi ili kuongeza ufanisi wa taasisi.

Waziri Mbarawa ameitaka TAA kuboresha huduma kwa wateja, kuimarisha uwazi na usalama wa viwanja vya ndege kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, kusimamia miradi kwa weledi na kuhakikisha matumizi sahihi ya teknolojia na ubunifu katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma.

Aidha, amebainisha changamoto za mapato zinazoikabili TAA, ikiwemo utegemezi wa ada za anga na gharama kubwa za uendeshaji, na kusisitiza umuhimu wa kubuni vyanzo vipya vya mapato kupitia uwekezaji wa ardhi, huduma za kidijitali, maegesho, huduma za abiria, mizigo na ubia na sekta binafsi (PPP).

Prof. Mbarawa ametoa rai kwa Uongozi wa  TAA kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa wafanyakazi ili kuongeza motisha na tija kazini.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Abdul  Mombokaleo, alieleza kuwa mkutano huo wa siku mbili, tarehe 18 na 19 Desemba, 2025 unahusisha wajumbe 107 na waalikwa 51 kwa lengo la kujadili masuala ya ustawi wa wafanyakazi na maendeleo ya taasisi.

Alibainisha kuwa TAA ina jumla ya watumishi 1,141 wa kudumu ,watumishi wa mikataba na wale  waliokopeshwa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama.

Aidha, alieleza mafanikio ya ukusanyaji wa mapato ya shilingi bilioni 163.97 kwa mwaka wa fedha 2024/25 na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa viwanja vya ndege ,miundombinu yake na kutaja changamoto za upatikanaji wa fedha na ucheleweshaji wa fidia huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau.