Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi azindua jengo la viongozi mashuhuri airport Dar.

Imewekwa: 16 Jan, 2026
Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi azindua jengo la viongozi mashuhuri airport Dar.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amezindua Jengo la Viongozi Mashuhuri (Presidential Pavilion) lililopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam, na kusema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na huduma za usafiri katika viwanja vya ndege, usafiri wa barabarani, majini na njia za reli, ili kuboresha huduma hizo nchini.

Dkt, Nchimbi amezindua jengo hilo leo January 16, 2026 ambapo amesema, Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ukamilishaji wa mradi huo wa jengo hilo.

Amesema ukamilifu wa ujenzi wa jengo hilo utazidi kukuza taswira ya taifa na kuimarisha diplomasia, itifaki na mahusiano ya kimataifa ambapo pia ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kusimamia jengo hilo na kulitunza ipasavyo ili kuboresha ubora na viwango vyake.

"Serikali imejizatiti kuhakikisha sekta ya uchukuzi inaimarika kwa ufanisi katika huduma kwani uchukuzi unaiweka nchi yetu kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara, Serikali ya awamu ya sita imejipanga vizuri kutekeleza miradi mbalimbali ya kisekta kama ilivyoainishwa katika dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050" amesema Makamu wa Rais Dkt. Nchimbi.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha inawezesha utekelezaji wa miradi iliyopangwa hatua iliyopelekea mradi huo kukamilika kwa wakati na kuchochea kuimarika kwa huduma za Viongozi Wakuu wa Nchi watakaoitembelea Tanzania na hivyo kuliletea heshima Taifa.

"Kwa sasa, Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa Kiwanja kipya cha Kimataifa cha Msalato, Ukarabati na uboreshaji wa Viwanja vya Ndege  vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Shinyanga, Sumbawanga, Tabora, Kigoma, Lake Manyara, Tanga, Iringa na Musoma, katika kuhakikisha inaendelea kuimarisha shughuli za utalii, biashara na kilimo, Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inaendelea na hatua za Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa Viwanja vipya vya Serengeti, Kyabajwa na Njombe" amesema Profesa Mbarawa