Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AAGIZA WIZARA ZA UCHUKUZI KUKUTANA NA SML AWARDS

Imewekwa: 25 Oct, 2026
MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AAGIZA WIZARA ZA UCHUKUZI KUKUTANA NA SML AWARDS

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amezitaka Wizara za Uchukuzi za Tanzania Bara na Zanzibar kukutana na uongozi wa SML Awards ili kuandaa mpango wa pamoja wa kutatua changamoto zinazowakabili wadau wa usafirishaji nchini.

Mheshimiwa Othman alitoa agizo hilo katika hafla ya utoaji tuzo kwa wasafirishaji na wadau wa sekta hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Superdome, Dar es Salaam, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Mheshimiwa Othman amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa huduma, kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Kihenzile, ambaye alimuwakilisha Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi umeleta matokeo chanya, hususan katika Bandari ya Dar es Salaam, iliyohudumia tani milioni 32.48 za mizigo mwaka wa fedha 2024/25 ikilinganishwa na tani milioni 17.8 mwaka 2021/22

Mheshimiwa Kihenzile ameongeza kuwa ongezeko hilo limechangiwa na maboresho ya miundombinu, matumizi ya teknolojia na ushiriki wa sekta binafsi, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia marekebisho ya sheria na sera.

Mkurugenzi Mtendaji wa SML Awards, Amoni Mtomyi, alisema tuzo hizo zinalenga kutambua mchango wa wadau wa ugavi, usafirishaji na lojistiki, pamoja na kuwakutanisha Serikali na sekta binafsi kujadili changamoto na kutafuta suluhisho la pamoja.