BAHI KUWA KITOVU CHA UHAMISHAJI MIZIGO KWA RELI – PROFESA MBARAWA
Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imezitaka TPA, TRC na TASAC kushirikiana kuboresha usafirishaji wa mizigo kwa reli ili kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na barabara za jiji hilo.
Akizungumza alipotembelea Kituo cha Bahi mkoani Dodoma, Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, amesema kituo hicho kinaongeza ufanisi kwa kuwezesha mizigo kutoka reli ya kisasa (SGR) kuhamishiwa kwenye reli ya zamani (MGR) kuelekea maeneo ambayo SGR bado haijafika.
Waziri Prof. Mbarawa amesema treni za mizigo kutoka Dar es Salaam hufika Bahi kwa takribani saa tano, huku Bandari ya Dar es Salaam ikihudumia zaidi ya makasha 3,000 kwa siku, hali inayohitaji kuimarishwa kwa njia mbadala za usafirishaji.
Waziri Profesa Mbarawa amezitaka taasisi hizo kushirikiana na wadau kuweka utaratibu utakaowawezesha wateja kukamilisha nyaraka na malipo ya mizigo katika vituo vya ndani, pamoja na kujifunza uzoefu wa nchi nyingine, ikiwemo Misri.
Pia ameipongeza TRC kwa kuanzisha uhamishaji wa mizigo kati ya SGR na MGR katika Kituo cha Bahi, akisema hatua hiyo itawezesha mizigo kuendelea na safari bila kusubiri ujenzi wa SGR kufika Isaka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Machibya Masanja, amesema huduma za SGR zinaendelea kuimarika, huku idadi ya abiria waliohudumiwa kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu ikifikia milioni 7.6. Kituo cha Bahi kinaendelea kuwa kiungo muhimu cha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya reli hizo mbili.
