MAADHIMISHO YA WANAWAKE SEKTA YA USAFIRI MAJINI YAFANYIKA KITAIFA KISIWANI UNGUJA
Katika kuadhimisha Siku ya wanawake walio katika sekta ya Usafiri Majini (Women in Maritime) iliyofanyika leo tarehe 18 Mei, 2024 katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil Zanzibar Mgeni Rasmi Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed amewapongeza wanawake wote kwenye sekta ya Usafiri Majini kwa kujitahidi kutimiza majukumu yao licha ya changamoto kadhaa wanazozikabili.
"Napenda kuwapongeza sana wanawake wote kwenye sekta ya Usafiri Majini kwa kujitahidi kutimiza majukumu yao licha ya changamoto kadhaa mnazozikabili. Jitihada zenu tunaziona na natambua kuwa, maadhimisho haya yanaenda kuleta hamasa katika kufikia lengo ya uchumi wa bluu Nchini na Duniani kote." Amesema Mhe. Dkt. Khalid.
Aidha, Mhe. Dkt. Khalid amewashauri wanawake kutoridhika na utaalamu walionao bali waendelee kutafuta utaalamu zaidi ili kuikuza sekta ya Usafiri kwa njia ya Maji kwa kubeba taswira nzuri ya WOMESA na taifa kwa ujumla.
"Ushauri wangu kwenu msiridhike na utaalamu huu mlionao sasa, endeleeni kutafuta utaalamu wa juu zaidi ili Taifa liwe na wataalamu wanawake wa kutosha na wenye sifa zote zinazohitajika ili kuikuza sekta hii ya Usafiri Majini kwa kubeba taswira nzuri ya Umoja wa Wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya Usafiri majini katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) pamoja na kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania kwa kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, umakini na kulinda maslahi mapana ya umma kwa Watanzania (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar)." Aliongeza Mhe. Dkt. Khalid.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu "Fursa Salama: Wanawake kuchagiza kesho ya Usalama kwa njia ya Maji" yamefunguliwa rasmi leo tarehe 18 Mei, 2024 yameambatana na ufunguzi wa Klabu ya "Maritime Club" yenye Kauli Mbiu ya "Catch Them Young".
Katika kuendeleza Maadhimisho hayo tarehe 19 na 20 Mei, 2024 WOMESA watatembelea wafungwa wanawake waliopo Chuo cha Mafunzo na kutoa misaada mbali mbali kwa Wafungwa hao, pia watatembelea shule ya Mikunguni, Lumumba na Al-Ihsan kwa ajili ya kuwahamasisha vijana kuhusu fursa za masomo ya sayansi ili waweze kupata nafasi za kusomea masuala ya sekta ya Usafiri Majini na fursa zilizopo, pamoja na kugawa vitabu vya kiada kupitia mradi wake wa Catch Them Young.
Siku ya Wanawake walio katika sekta ya Usafiri Majini (Women in Maritime) ilianza kuadhimishwa rasmi kwa mara ya kwanza mwaka 2022.