Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

MAADHIMISHO YA KWANZA YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI 2025 YAHITIMISHWA RASMI

Imewekwa: 30 Nov, 2025
MAADHIMISHO YA KWANZA YA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU ARDHINI 2025 YAHITIMISHWA RASMI

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Uchukuzi kwa niaba ya Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara, leo  tarehe 29 Novemba, 2025 amefunga rasmi Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025 yaliyofanyika  kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, na kusisitiza dhamira ya Serikali kuendeleza mifumo ya usafiri iliyo salama, rafiki kwa mazingira na inayokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo yaliyodumu kuanzia Novemba 24 hadi 29, Kaimu Katibu Mkuu amesema Serikali imejipanga kuharakisha maboresho ya miundombinu, matumizi ya nishati safi, na teknolojia bunifu ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri wa ardhini.

“Maadhimisho haya yametoa dira mpya, tumepokea maoni,Ubunifu na suluhisho kutoka kwa wadau mbalimbali, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha mfumo wa usafiri unakuwa wa kisasa, salama, wenye gharama nafuu na unaolinda mazingira” amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo ameelezea mafanikio ya maadhimisho haya na kusisitiza kuwa yaliambatana na vipindi vya kujenga uwezo kwa wadau.

“Maadhimisho haya yenye kaulimbiu ya ‘ Nishati safi na ubunifu katika usafirishaji’ yaliambatana na siku tatu za mafunzo, elimu na mijadala ya wazi iliyofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC), ambapo tulipokea mada kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje, ambazo zimeongeza uelewa kuhusu nishati safi, usalama barabarani na mustakabali wa usafiri endelevu nchini” amesema

Ameongeza kuwa LATRA itaendelea kusimamia kikamilifu ubora wa huduma, kutumia mifumo ya kidigitali, kuongeza elimu kwa watoa huduma na abiria, na kuhakikisha ubunifu unaozingatia usalama na ulinzi wa mazingira unatekelezwa kwa vitendo.

Maadhimisho haya yamehitimisha Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025 ambayo kwa mara ya kwanza imeunganisha Serikali, wadau, wananchi na wabunifu katika kujenga taifa lenye mfumo wa usafiri wa kisasa, salama na rafiki kwa mazingira ambapo maonesho yajayo yanatarajiwa kufanyika tarehe 23-28 Novemba, 2026