KONGAMANO LA KITAIFA LA WADAU WA UCHUMI WA BULUU LAFUNGWA RASMI JIJINI DAR ES SALAAM

Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu limehitimishwa rasmi leo, Septemba 11, 2025, katika Hoteli ya King Jada, Morocco Square, jijini Dar es Salaam.
Akifunga rasmi kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amesisitiza dhamira ya Serikali katika kuendeleza uchumi wa buluu kupitia uwekezaji mkubwa unaofanywa kwenye sekta ya uchukuzi, hususan upande wa bahari na bandari.
“Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa majini, ikiwemo ununuzi wa gati mpya kwa ajili ya wavuvi. Ni wajibu wenu kama wadau kuhakikisha maazimio ya kongamano hili yanatekelezwa kwa vitendo. Ninyi ndiyo nguzo muhimu (pillars) za kusukuma mbele dira ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2050,” alisema Prof. Kahyarara.
Akizungumza Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gulumo, alieleza kuwa maadhimisho haya yameweka msisitizo kwa wadau kuandaa mipango ya sera na matumizi sahihi ya rasilimali za bahari kwa maendeleo endelevu. Aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kuweka mkazo kwenye Mpango wa elimu ya uchumi wa buluu kwa wadau mbalimbali, Utoaji wa elimu kwa vijana waliopo mashuleni na vyuoni, Ulinzi na usalama wa maeneo ya maji, Na kuandaa tafiti makini zinazolinda mazingira ya baharini.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais alitoa salamu za shukrani kwa Niaba ya katibu mkuu na wafanyakazi wote toka upande wa Bara, akieleza matumaini kuwa mijadala iliyofanyika itazaa matokeo chanya kwa taifa.
Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia DMI, na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi – Zanzibar. Lengo kuu ni kuunganisha wadau kutoka sekta mbalimbali na kuweka mikakati ya kitaifa ya kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia shirikishi na endelevu.