Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

*KONGAMANO LA KITAIFA LA WADAU WA UCHUMI WA BULUU LAANZA RASMI DAR ES SALAAM*

Imewekwa: 15 Sep, 2025
*KONGAMANO LA KITAIFA LA WADAU WA UCHUMI WA BULUU LAANZA RASMI DAR ES SALAAM*

Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu limeanza leo katika Hotel ya  King Jada iliyopo kwenye majengo ya  Morocco Square, jijini Dar es Salaam na linatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo hadi kesho Septemba 11, 2025.

Akizidua kongamano hilo Mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais,Bw.Abdallah Mitawi, amesema Serikali imedhamiria kutumia fursa kubwa za rasilimali za bahari na maji ya ndani kwa maendeleo endelevu ya Taifa. “Uchumi wa buluu ni injini mpya ya maendeleo ya Tanzania, ukitumiwa ipasavyo unaweza kuongeza ajira, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa wananchi,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi Mha. Shomari Shomari amebainisha kuwa maboresho  ya miundombinu ya bandari, reli na vyombo vya usafirishaji majini ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa buluu na kuongeza ushindani wa biashara ndani na nje ya nchi na kusisitiza umuhimu wa  ushirikiano wa wadau wote katika kuhakikisha miradi ya usafirishaji inazaa matunda kwa Taifa.

Aidha, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI)  Prof. Tumaini Gulumo alieleza majukumu ya chuo hicho katika kutoa elimu na tafiti za bahari pamoja na kuzalisha wataalamu wanaohitajika kwenye sekta ya bahari, usafirishaji na uhifadhi wa mazingira ya pwani.

Amesema DMI ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi wa buluu kwa kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu kwenye sekta hiyo.

Kongamano hili limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia DMI, na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi – Zanzibar, likiwa na lengo la kuunganisha wadau wote muhimu na kuweka mikakati ya kitaifa ya kuendeleza uchumi wa buluu kwa njia endelevu.