KIWANJA CHA NDEGE SUMBAWANGA KUCHAGIZA MAENDELEO
Uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga umeelezwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Rukwa na maeneo jirani, kufuatia kuanza rasmi kwa uendeshaji wake Aprili 24, 2026.
Akizindua uwanja huo kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya usafiri wa anga ili kuboresha huduma, kuunganisha mikoa na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri huku ikifungua maeneo yenye fursa mbalimbali za maendeleo, na kuongeza kuwa uwanja huo utachochea ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo amesema ujenzi wa uwanja huo umegharimu shilingi bilioni 62.1 na unajumuisha miundombinu muhimu ikiwemo barabara ya kuruka na kutua ndege, jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia hadi abiria 150,000 kwa mwaka pamoja na huduma za hali ya hewa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema kampuni hiyo imejipanga kuanza safari za ndege mara mbili kwa wiki katika mkoa huo, hatua itakayorahisisha usafiri wa abiria na mizigo pamoja na kukuza biashara, utalii na uwekezaji.
Akitoa salamu za mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Msalike Makungu, amesema uzinduzi wa uwanja huo utafungua fursa kubwa za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.
