KIPANDE CHA RELI YA SGR KUTOKA BANDARINI KUUNGANISHWA NA NJIA KUU KUMALIZA MSONGAMANO BANDARI YA DAR ES SALAAM
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa kipande cha awamu ya kwanza cha Reli ya Kisasa (SGR) kitakachotengeneza njia na kuingia na kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda kuungana na njia kuu ya SGR kuelekea Dodoma na Mikoa mingine nchini kwa ajili ya mizigo ni hatua muhimu katika kupunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi wa upakuaji na usafirishaji wa shehena bandarini.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo la ujenzi lililopo Malindi Yard Jijini Dar es salaa leo tarehe 28 Novemba,2025 Prof. Mbarawa amesema kipande hicho ni muhimu kwa sababu kitawezesha mizigo ya makontena kutoka bandarini kuingia moja kwa moja kwenye njia kuu ya reli kwenda Dodoma na maeneo mengine, kinyume na ilivyo sasa ambapo mizigo husafirishwa kupitia Pugu kabla ya kuunganishwa na SGR.
Amesema kipande kilichobakia cha kilomita 2.5 kiko katika hatua za mwisho, ambapo nyaya za umeme na maandalizi ya njia yamekamilika kwa kiwango kikubwa ili kuruhusu mizigo kusafirishwa kwa urahisi kutoka bandari hadi kwenye reli kuu na itakamilika hivi karibuni.
“kazi hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Januari 2026, ambapo TRC itasimamia ununuzi wa mafuta, chuma na vifaa vingine muhimu huku mkandarasi akiendelea na usimamizi wa ujenzi, ili kuharakisha utekelezaji na kuepusha kucheleweshwa kwa mradi ili uanze kutumika haraka” amesisitiza Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema kukamilika kwa kipande hicho kutapunguza msongamano bandarini na kuongeza ufanisi wa utendaji, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuunganisha moja kwa moja reli ya kisasa hadi ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, hatua ambayo itawezesha meli kushusha mizigo kwa haraka, kuongeza mapato ya bandari na kuchochea uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TRC, Mha Tito Mateshi amesema ujenzi huo umefikia zaidi ya kilomita nne, huku kilomita 1.5 zikiwa zimebaki kukamilika na kutilia mkazo kuwa maandalizi ya tuta yameshakamilika katika maeneo mengi na wanatarajia ndani ya miezi miwili na nusu kazi ya sehemu ya upakiaji mizigo kukamilika.
