KIHENZILE AITAKA LATRA KUCHUKUA HATUA KWA MADEREVA WANAOCHEZEA MFUMO WA VTS
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile ameutaka Uongozi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha unawachukulia hatua za kisheria Madereva wanaochezea mfumo maalum wa kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS).
Naibu Waziri Kihenzile ameyasema hayo wakati alipotembelea ofisi ya LATRA jijini Dar es Salaam na kituo maalum cha Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) kilichopo Mikocheni Jijini humo.
Naibu Waziri Kihenzile amesema pamoja na kuchukua hatua kwa madereva hao LATRA iongeze nguvu kwenye zoezi la kuwatahini madereva ili kupima umahiri wao katika utendaji kazi wawapo barabarani.
“Kuna baadhi ya Madereva wa Mabasi wanaochezea Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na wanafanya hivi wakati mwigine wamiliki wa mabasi hayoa hawajui kama kuna mchezo wa namna hiyo unafanyika hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa kila dereva anayechezea mfumo”. Amesema Mhe. Kihenzile.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya LATRA Prof. Ahmed Mohamed Ame, amesema maboresho mbalimbali katika mfumo huo yameendelea kufanyika ambapo kwa sasa mfumo unaweza kutengeneza namba za malipo na kuzipeleka moja kwa derevea aliyevunja sheria.
Mwenyekiti Prof. Ame amoengeza kuwa LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha madereva wanafuata kanuni na taratibu zote za Usalama barabarani wawapo safarini.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara kutoka LATRA Johansen Kahatano amesema madereva takribani 2757 wameshafanya mtihani wa kuthibitishwa na LATRA ambapo kati ya hao madereva takribani 1817 wamefaulu.
Naibu Waziri Kihenzile yuko jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukauga miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara ya Uchukuzi.