Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

KATIBU MKUU UCHUKUZI PROF. KAHYARARA AFUNGA WARSHA YA ICAO JIJINI DAR ES SALAAM

Imewekwa: 02 Mar, 2026
KATIBU MKUU UCHUKUZI PROF. KAHYARARA AFUNGA WARSHA YA ICAO JIJINI DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amefunga rasmi Warsha ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) kuhusu Mikataba ya Sheria za Anga ya mwaka 2026, akisema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa warsha hiyo kubwa ya kimataifa iliyowakutanisha wadau wa sekta ya usafiri wa anga kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Prof. Kahyarara alisema hayo Februari 26, 2026, jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa kufanyika kwa warsha hiyo nchini ni ushahidi wa imani kubwa ya jumuiya ya kimataifa kwa Tanzania. Alisema hali hiyo inatokana na misingi imara ya amani, utulivu na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta mbalimbali, ikiwemo usafiri wa anga.

“Tanzania imeendelea kuwa mahali salama pa kufanyia mikutano mikubwa ya kimataifa. Haya yote ni matunda ya amani tuliyonayo pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.” alisema Prof. Kahyarara.

Aliongeza kuwa warsha hiyo imeongeza uelewa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika eneo la sheria za anga, jambo litakalosaidia nchi kujiandaa vyema kukabiliana na changamoto pamoja na kutumia fursa mpya za teknolojia katika usafiri wa anga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi, alisema warsha hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na imefungua ukurasa mpya wa mageuzi ya kisheria ndani ya sekta ya anga nchini.

Bw. Msangi alisema kupitia majadiliano ya siku mbili, Tanzania imepata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa kimataifa, kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ya haraka, pamoja na kutoa mchango wa moja kwa moja, hususan katika uridhiaji na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya anga.

Alisisitiza kuwa TCAA itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa ili kuhakikisha sheria na mifumo ya anga ya Tanzania inaendana na viwango vya kimataifa, sambamba na kuhakikisha usalama, ufanisi na uendelevu wa sekta ya usafiri wa anga nchini.

Aidha, ilielezwa kuwa warsha hiyo ni ya tatu kufanyika duniani na ya kwanza kufanyika barani Afrika, ambapo Tanzania imepata bahati ya kuwa mwenyeji wa tukio hilo muhimu la kimataifa.

Warsha hiyo imeandaliwa na TCAA kwa kushirikiana na ICAO.