Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

KAMATI YASISITIZA USIMAMIZI MRADI WA BANDARI YA KILWA MASOKO

Imewekwa: 20 Nov, 2023
KAMATI YASISITIZA USIMAMIZI MRADI WA BANDARI YA KILWA MASOKO

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso amezitaka Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana kumsimamia mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa bandari ya Kilwa Masoko Mkoani Lindi ili ukamilike kwa wakati na viwango.

 

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo  mkoani Lindi Mwenyekiti Kakoso amesema bila kuwa na mkakati madhubuti wa usimamizi kwenye ngazi zote za utekelezaji thamani ya fedha haitoonekana baada ya mradi kukamilika hivyo kazitaka Wizara hizo kuongeza nguvu kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara.

 

“Serikali inatoa fedha nyingi katika kutekeleza miradi lakini changamoto iliyopo wakandarasi wanaotekeleza miradi hii hawasimamiwi kwa karibu sasa nyinyi mna wataalam wa kutosha waleteni hapa wakague kazi zinazoendelea kila siku maana  tunataka kuona thamani ya fedha zilizowekezwa kwenye mradi huu’ amesema Mwenyekiti Kakoso.

 

Mwenyekiti Kakoso amesema pamoja na ujenzi huo Wizara hizo zihakikishe miradi ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) iliyopangwa kutekelezwa inazingatia mahitaji ya wahusika ili wananchi wapate manufaa zaidi kwenye maeneo nje ya uwekezaji huo wa bandari.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David Kihenzile amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha wavuvi kufanya biashara kwa urahisi kwani umezingatia mahitaji yote ikiwemo miundombinu ya kutunzia na kuhifandhi  bidhaa za Samaki kabla ya kusafirishwa kwa watumiaji wa ndani na nje ya Nchi.

 

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi  Juma Kijavara amemuhakikishia Mwenyekiti Kakoso tayari TPA imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba.

 

Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Wilayani Kilwa unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilion 250 na unatarajiwa kukamilika Februari, 2025 ambapo kukamilika kwake kutaifanya Tanzania kuwa na Bandari ya kwanza ya uvuvi ambayo itakuwa kichocheo cha uchumi, kuongeza ajira na upatikanaji wa Samaki wa lishe na kuongeza mapato ya Serikali.