KAMATI YAPONGEZA MRADI WA KIWANJA CHA MSALATO
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeipongeza Wizara ya Uchukuzi kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Msalato jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mradi huo leo, Mwenyekiti wa kamati hiyo Seleman Kakoso amesema wamerishishwa na jitihada za serikali katika ujenzi wa kiwanja hicho.
"Pamoja na mafanikio yaliyopo tunaiomba serikali iwasilishe kwa maandashi maelezo kuhusu sababu za kuongezeka kwa gharama za ujenzi wa mradi ili kamati ipate taarifa kwa uzuri," Amesema Kakoso.
Aidha Kakoso ameiomba serikali kuhakikisha inatekeleza kile ambacho TAA inashauri pamoja na Shirika la Kimataifa la Usafiriwa Anga (ICAO) ili kuwa kiwanja kinafikia viwango vinavyotakiwa pamoja na kuepuka kasoro siku za usoni bqada ya mradi kukamilika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema kuwa mradi umefikia asilimia 90 kwa upande wa miundombinu na asilimia 80 kwa upande wa majengo.
Pamoja na hayo Kihenzile amesema serikali imepokea na itaendelea kupokea ushauri wa kamati utakaotolewa kuhusu mradi huo ili uweze kuwa na ubora unaotakiwa.
