Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

KAMATI YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA KUKAMILIKA UKARABATI MV. LIEMBA

Imewekwa: 17 Aug, 2026
KAMATI YA MIUNDOMBINU YAPONGEZA KUKAMILIKA UKARABATI MV. LIEMBA

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu imeipongeza serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kufanikisha ukarabati wa wa Meli ya MV Liemba chini ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kufuatia majaribio yaliyoanza kufanyika Tarehe 15 Agosti 2026.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso ametoa pongezi hizo katika kikao cha Kamati kilichofanyika leo bungeni jijini Dodoma, kilichokuwa na lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utendaji wa Shirika la SINOTASHIP na taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Meli ya MV Liemba.

"Naomba kabla ya kuanza rasmi kwa meli ya MV Liemba mkashughulikie suala la wafanyakazi maana tunajua wengi wamestaafu na wengine waliondoka baada ya meli kusimama kufanya kazi," Amesema Kakoso.

Pamoja na mambo mengine amelitaka shirika la SINOTASHIP kujiendesha kibiashara ili liweze kutumia kwa ufanisi fursa zilizopo katika eneo la bahari ili kuzalisha faida kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji nchini kwa kuzingatia faida kubwa tuliyonayo kijiografia.