Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

JENGO LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE WA TABORA KUANZA KAZI – MBARAWA

Imewekwa: 21 Nov, 2025
JENGO LA ABIRIA UWANJA WA NDEGE WA TABORA KUANZA KAZI – MBARAWA

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amekagua na kutembelea jengo la uwanja wa ndege ambao ujenzi wake umefikia asilimia 98 ambapo ameonyeshwa kuridhishwa na maendeleo hayo.

Jengo hilo la kisasa, lililojengwa na Serikali kwa gharama shilingi bilioni 27.93, linatarajiwa  kuhudumia abira 120 kwa wakati mmoja kwa ujumla jengo hilo lina maduka.     

"Nimechagua kuanza ziara yangu Tabora kwa sababu ni mkoa wa kimkakati. Reli kutoka Makutupora hadi Tabora, Isaka, Mwanza, na Tabora hadi Uvinza, Bunjumbura hadi Congo – zote zinaifanya Tabora kuwa kitovu cha usafirishaji wa kimataifa." Amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo la abiria ni hatua muhimu kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, akimuwakilisha mkuu wa mkoa wa tabora Pendo Wella, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mradi huo mkubwa, akiahidi kuwa Serikali mkoa na wananchi watautunza ipasavyo na kuhakikisha unaleta fursa za kiuchumi kwa wakazi na wawekezaji wa Tabora.

Aidha Mhandisi wa mradi huo, Raphael Stanislaus Mlimaji, ambaye ni meneja wa tanroad mkoa wa tabora amesema jengo hilo lina uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja, lina ofisi za idara mbalimbali, maeneo ya biashara, mnara wa kuongozea ndege, mifereji, eneo la maegesho ya magari (magari 54 kwa wakati mmoja), uzio wa usalama wa urefu wa km 6.25, kituo cha hali ya hewa, majenereta mawili (1000kva na 40kva), taa za sola, pamoja na transfoma ya 1250KVA.