HANGAR YA NIT KUIMARISHA MAFUNZO YA ANGA
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kutunzia na kukarabati ndege (Hangar) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), mradi unaotekelezwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Mradi huo wenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 5 umefikia zaidi ya asilimia 80 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Novemba 2026.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo mkoani Kilimanjaro, Naibu Waziri Kihenzile amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya mafunzo ya anga ili kuongeza upatikanaji wa wataalamu wenye ujuzi na kukidhi mahitaji ya sekta hiyo.
Naibu Waziri Kihenzile ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza idadi ya wataalamu wazawa wa anga, kuimarisha uwezo wa ndani katika matengenezo ya ndege na kupunguza utegemezi wa wataalamu na huduma kutoka nje ya nchi, sambamba na kuongeza fursa za ajira na kuchangia ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga na uchumi wa Taifa.
Naye Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema Hangar hiyo itaimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosomea urubani na ufundi wa ndege, kwa kuwa itawapa fursa ya kujifunza katika mazingira yanayofanana na maeneo halisi ya kazi.
“Mradi huu utaongeza uwezo wa Chuo kutoa mafunzo yanayozingatia vitendo zaidi, jambo litakalowajengea wanafunzi umahiri unaohitajika katika soko la ajira la sekta ya usafiri wa anga,” amesema Dkt. Mgaya.
Dkt. Mgaya amesema kuwa wanafunzi watapata fursa ya kufanya mazoezi ya ukaguzi, matengenezo na utunzaji wa ndege chini ya usimamizi wa wataalamu, hatua itakayowawezesha kuhitimu wakiwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza ushindani wao ndani na nje ya nchi.
Dkt. Mgaya ameongeza kuwa uwekezaji huo utaongeza uwezo wa NIT kutoa mafunzo yanayokidhi viwango na mahitaji ya sekta, huku ukichochea matumizi ya teknolojia za kisasa katika ufundishaji.
