Burundi kuunganishwa na Tanzania kwa reli ya Kisasa ya SGR

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa , amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway – SGR) kipande cha Uvinza (Tanzania) hadi Musongati (Burundi), Lot 7&8, iliyofanyika leo Tarehe 16 Agosti,2025 katika eneo la Musongati, nchini Burundi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye, ambaye alikuwa mwenyeji wa tukio hilo na Viongozi wa Serikali, Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Wadau wa Maendeleo na Wananchi wa pande zote mbili.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia, Waziri Mkuu Majaliwa amesema mradi wa reli ya kisasa ni uthibitisho wa mshikamano wa muda mrefu wa Nchi hizi mbili ulioanza toka mwaka1975 na ni ajenda ya mwaka 2063,
Amesema mradi huu utarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa gharama nafuu na kuongeza ushindani wa kiuchumi kikanda
"Reli hii ni injini mpya ya uchumi wetu na ni Reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi kikanda " amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Mhe. Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa mradi huo.
"Reli hii itafungua fursa mpya za kibiashara, kuongeza ajira, na kuimarisha mshikamano wa kikanda, ni hatua kubwa kuelekea mustakabali wa ustawi wa watu wetu," amesema Rais Ndayishimiye.
Naye Waziri Mkuu wa Burundi Mhe.Nestor Ntahontuye Amesema reli hii italeta mageuzi makubwa katika sekta ya usafirishaji na kufungua milango ya uwekezaji mpya nchini Burundi.
Aidha, Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia usafirishaji wa Mizigo wa madini ya Nikel kutoka Msongati ambao utapita Uvinza mpaka Bandari ya Dar es Salaam, ambapo itaunganisha masoko ya ndani na kimataifa kwa gharama nafuu hivyo kuchochea maendeleo pande zote mbili.
Amesema reli hiyo itakuwa na urefu wa Km 300 ambapo 240 za njia kuu na Km 60 njia za mapishano itatumia nishati ya umeme ambayo ni rafiki wa mazingira, utatekelezwa na Mkandarasi kutoka China wa CRCG LTD kwa miezi 72.