Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA UCHUKUZI TRILIONI 2.872 KWA MWAKA WA FEDHA 2026/27

Imewekwa: 14 May, 2026
BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA UCHUKUZI TRILIONI 2.872 KWA MWAKA WA FEDHA 2026/27

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 13 Mei, 2026 limeidhinisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi yenye jumla ya Shilingi Tril. 2.872 kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kuendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuboresha huduma za usafiri.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kati ya fedha zilizoidhinishwa, Shilingi Bil. 126.041 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi Tril. 2.746 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Waziri Mbarawa amesema kuwa vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2026/27 ni pamoja na kuendelea na ujenzi na uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR, ukarabati na uboreshaji wa reli za MGR na TAZARA, uboreshaji wa miundombinu ya bandari, usafiri wa anga, ujenzi na ukarabati wa meli pamoja na kuboresha huduma za hali ya hewa na vyuo vya mafunzo vya kisekta

Ameongeza kuwa, Katika sekta ya bandari, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP) pamoja na maboresho ya bandari mbalimbali za mwambao wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu zikiwemo Bandari za Bagamoyo, Mtwara, Mwanza North, Mbamba Bay na Kigoma

Aidha, Serikali imeeleza kuwa kupitia ushirikiano na sekta binafsi, maboresho makubwa yanaendelea katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo uwekezaji wa vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo umeongeza na utaendelea kuongeza ufanisi, ushindani na uwezo wa kuhudumia shehena mbalimbali bandarini

Amesema  kwa upande wa usafiri wa anga, Wizara itaendelea na ununuzi wa ndege na kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga pamoja na ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini ikiwemo Mwanza, Arusha, Mtwara, Serengeti, Kagera, Kilimanjaro na Julius Nyerere.

Zaidi ya hayo, amesema katika sekta ya reli, Serikali itaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, ukarabati wa reli za MGR na TAZARA pamoja na kuanza upembuzi yakinifu wa mradi wa treni ya mjini katika Jiji la Dar es Salaam.