Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

ATCL YAREJESHA SAFARI ZA NDEGE MKOANI IRINGA-WAZIRI MBARAWA

Imewekwa: 22 Feb, 2025
ATCL YAREJESHA SAFARI ZA NDEGE MKOANI IRINGA-WAZIRI MBARAWA

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan imerejesha Safari za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) zilizokua zimesimama takribani miaka mitano (tangu mwezi Juni 2020).

Urejeshwaji wa safari hizo za ndege umefuatia kukamilika kwa Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa uliogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 63.742.

Ukarabati na Upanuzi wa Uwanja huo umefanywa na Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Mamlaka  ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ambapo hivi sasa Uwanja umekamilika asilimia 95 hivyo kuwezesha kuanza rasmi Safari za Ndege za ATCL mara tatu kwa wiki

Maelezo hayo ya Serikali yametolewa leo na Mhe. Prof Makame Mbarawa, Waziri wa Uchukuzi wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Safari za Ndege kati ya Dar es Salaam na Iringa iliyofanyika leo tarehe 22 Februari 2025 Mjini Iringa mara baada ya kutua kwa mara ya kwanza kwa ndege ya ATCL tangu ilipofanya safari zake mara ya mwisho mwaka 2020.

Kurejeshwa kwa safari hizi, kutasaidia kupunguza muda wa safari kati ya Iringa na Dar es Salaam, kuchochea uwekezaji, na kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje wanaotembelea vivutio vya Iringa kama vile Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Hii ni hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa huduma za usafiri wa anga zinapatikana kwa ufanisi na kwa gharama nafuu, “Profesa Mbarawa”