Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Uchukuzi

SEKTA BINAFSI KUCHOCHEA UWEKEZAJI WA UCHUKUZI KWA ASILIMIA 70 KUELEKEA DIRA 2050

Imewekwa: 20 Nov, 2026
SEKTA BINAFSI  KUCHOCHEA UWEKEZAJI WA UCHUKUZI KWA ASILIMIA 70 KUELEKEA DIRA 2050

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amezitaka taasisi za uchukuzi kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo ili kuongeza uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati

Akizungumza jijini Mwanza wakati wa kufunga Mkutano wa 19 wa Mapitio ya Pamoja ya Sekta ya Uchukuzi (JTSR) tarehe 17 Nov, 2026, Dkt. Mkama amesema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya rasilimali fedha za utekelezaji wa Dira 2050, hivyo ni muhimu kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, hususan kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP)

Amezitaka Wizara, idara, wakala na taasisi za umma kutekeleza kwa vitendo maazimio ya mkutano huo. Akielezea mafanikio ya sekta ya uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, amesema Reli ya Kisasa (SGR) ilisafirisha abiria mil. 3.53 dhidi ya lengo la mil. 3.05, sawa na kuvuka lengo kwa asilimia 15.96

Katika sekta ya anga, idadi ya abiria iliongezeka kutoka mil. 7.53 hadi mil. 8.36, huku mizigo ikipanda kutoka tani 41,022.7 hadi tani 45,149.0. Aidha, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lilipanua mtandao wake wa safari kutoka vituo 27 hadi 35. Katika sekta ya barabara, Serikali imekamilisha ujenzi wa kilomita 24 za barabara ya Rudewa–Kilosa, huku miradi ya barabara ya mzunguko wa Dodoma na Daraja la Jangwani ikiendelea

Akitoa salamu za Wizara kwa niaba ya katibu mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof.Godius Kahyarara, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini Bi Devota Gabriel, amesema mkutano huo umebainisha mafanikio na changamoto za kisekta, hususan matengenezo ya miundombinu iliyopo. Ameeleza kuwa hoja na maazimio yaliyoibuliwa yatafuatiliwa kupitia Hati ya Makubaliano ya Pamoja (Aide Memoire) itakayotiwa saini na washirika wa maendeleo pamoja na makatibu wakuu wa sekta husika

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema sekta za Uchukuzi na Ujenzi zinategemeana katika kukuza uchumi, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mtandao wa barabara ili kuunganisha miundombinu ya reli, bandari na viwanja vya ndege na kuongeza tija ya uwekezaji.